![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEibmNX4sJD5fVqlpPsUQ7rBCFyPfmjMI4FfoA34VO2IB6qWta7dHVDm8jNJ0u75dHLlQDSsrjZjDu8Mk362dLoVGnGfpfub9BMXggy6ADkpgvkNnUsluWc4Bpd_D8od1tqNcNhY8kcj9OPG/s320/jose-mourinho+345.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjWX4UWVe6oTWPoPTgvUiOrsn8yxTxNMgQ49aU4jUT9GITaVCEWbCSb-VEc1KqXG1l1C_erENd1V-CTHGubNSm9LmYxCda4MYipqMdTSquUOLWhabzaR-n0GkZmb41kcbWGNjfjywEYzgUd/s200/P_Jose_Mourinho_3_01.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjr8eIL8ac6lDNU_hCx71C4jxtq96nqerzv4UU5zg9Y1SfwLPi-MowMktSceqitIP0DRdFiZnaUECuBGu7R6XOGeYlAyDnQY50mgWI-ksUn-n3nS55FqoYu_BbHtK1VaF3Ph4l3wBjx5jCU/s200/Jose_Mourinho-07.jpg)
![](file:///C:/DOCUME%7E1/user/LOCALS%7E1/Temp/moz-screenshot-3.jpg)
A-Z MOURINHO ALIVYOITEMA CHELSEA
London, England Kocha Mkuu wa ChelseaThe Blues ya England, Jose Mourinho (44) amejiuzulu kuifundisha timu hiyo yenye makazi yake jijini London.
Mourinho aliyejiunga na Chelsea akiwa kocha mkuu, June 2, 2004, akitokea Futebol Clube do Porto (FC. Porto) ya Ureno, aliachia ngazi Jumatano ya wiki hii, jambo lililoibua mshtuko mkubwa kwa mashabiki na uongozi mzima wa The Blues.
Vyanzo mbalimbali vya habari nchini humo, vilieleza kuwa hatua iliyochukuliwa na Mourinho ilitokana na mvutano uliokuwepo kati yake na mmiliki wa klabu hiyo, Mrusi Roman Abromovich.
Utata ulioibuka kati yake na Abramovich, ulichangia wawili hao kuishi kama chui na paka katika mbuga moja, taswira ambayo iliwafanya wachambuzi wa soka kumbashiria Mourinho kama mtu aliye mguu mmoja ndani mwingine nje kwenye himaya ya Stanford Bridge.
Habari za ndani ya Chelsea zilisema kwamba mvutano huo wa kocha na bosi wa klabu, ulifikia hatua mbaya licha ya kufanyika vikao kadhaa vya usuluhishi. Ilielezwa na vyanzo vya ndani ya klabu hiyo kuwa katika vikao hivyo, wawili hao walikubaliana kumaliza tofauti zao, ingawa Mourinho alibaki na nongwa.
Didier Deschamps ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, alisema kwamba hatua ya Mreno huyo ni sahihi kwakuwa uamuzi aliouchukua ni wa kijsiri, ingawa si busara kumsifu.
Najua hali ya Chelsea imefikia hatua mbaya, kwa maana hiyo, kocha alikuwa hana namna ya kufanya isipokuwa kuachia ngazi, huo ndiyo ukweli usiopingika. Nafikiri inajulikana wazi kuwa Mourinho ni miongoni mwa makocha bora na wenye kiwango bora katika ulimwengu wa sokaĆ alisema Deschamps.
Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Redio cha BBC, Jonathan Legard, alisema kuwa alifahamu kama kocha huyo atabwaga manyanga baada ya kupokea taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms), kutoka Mourinho akiwaambia wachezaji wake kuwa anasaini 'out'.
Wachezaji waliojulishwa na kocha wao juu ya mipango yake ya kutaka kutimka kupitia sms ni John Terry na Didier Drogbar ambao walikuwa watu wake wa karibu.
Baada ya kuwajulisha wachezaji hao, kocha huyo mwenye maneno mengi aliandika waraka kwenda kwenye Mejimenti ya Chelsea na nakala kuwatumia. Mkurugenzi Mtendaji, Peter Kenyon, Mwenyekiti Bruce Buck na Abramovich mwenyewe.
Wakati habari hizo zilipoanza kuenea, wakazi wa Jiji la London, baadhi viongozi wa ngazi za juu wa Chelsea na wachezaji wengine, walikuwa hawana taarifa kuhusu kuondoka kwa Jose Mourinho.
Ilielezwa kuwa muda mfupi kabla ya Mourinho kutangaza kung'atuka, baadhi ya viongozi, wachezaji na kocha huyo Mreno, walikutana kwenye tafrija iliyofanyika katika Jumba la Sinema la Fulham Broadway na kusherehekea mafanikio ya kimapinduzi ya klabu hiyo, waliyoyaita 'Blue Revolution'.
Kocha huyo aliingia kwenye jumba hilo akiwa amechelewa, lakini hakufanya mazungumzo yoyote na waandishi wa habari waliokuwa wamemsubiri ili kuzungumzia suala hilo kutimka, kwani tayari uvumi ulishaenea.
Kutokana na kujiuzulu ghafla kwa kocha huyo, Menejimenti ya Chelsea, ilikaa kikao cha dharura, kilichowahusisha Peter Kenyon, Bruce Buck, Roman Abramovich na Eugene Tenenbaum na kutathmini hali hiyo ambayo imewashtua wengi.
Kufuatia mabadiliko hayo, Kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Israel, Avram Grant ndiye anayetarajiwa kuchukua nafasi ya kusimamia dawati la ufundi la Chelsea wakati wa mechi ya Ligi Kuu, England, Jumapili dhidi ya Manchester United.
Avram Grant ni swahiba wa Abramovich na alikuwa hapikiki chungu kimoja na Mourinho ambaye alikuwa akimtuhumu kumpikia majungu kwa bosi wake. Katika msimu wa Ligi Kuu uliopita, 'The Blues' ilimaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Manchester United 'Mashetani Wekundu' lakini ilifuta machozi baada ya kushinda vikombe vya FA na Carling Cup.
Kumbu kumbu muhimu za Mourinho akiwa na Chelsea.
Juni 2 2004 - Aliwasili Stamford Bridge
Februari 27 2005 - Aliipa Kombe la Carling baada ya kuifunga Liverpool bao 3-2. Mei 4 2005 - Alisaini mkataba mpya wa miaka mitano.
Aprili 29 2006 - Aliibebesha ubingwa wa Ligi kuu kwa kuifunga Manchester United 3-0.
Februari 27, 2007 - Ushindi wa Kombe la Carling baada ya kuifunga Arsenal 2-1.
Mei 19, 2007 - Ushindi wa Kombe la FA kwa kuitandika. Man Utd 1-0 kwenye Uwanja wa Wembley.
Septemba 19, 2007 - Alivunja mkataba na kuondoka Stamford Bridge.
BAADA YA KUTOKA UNDANI NA KIINI KILICHOMTOA JOSE ANTONIO MOURINHO ENDELEA KUPATA HABARI NYINGINE ZA KUTOKA MAJUU, KATIKA SAFU YA VIMBWANGA VYA MASTAA DUNIANI.
Lerato wa BBA amwaga chozi live
Johnesburg, Afrika Kusini
Mshiriki wa Afrika Kusini katika Shindano la Big Brother Afrika 2007, Lerato, aliangua kilio hadharani, wakati mpenzi wake ambaye ni mshindani mwenzake kutoka Zambia, Maxwell, alipotangazwa kutolewa Jumapili iliyopita.
Lerato mwenye sifa ya kudeka, alimwaga chozi baada ya kubaini kwamba atamkosa mpenzi huyo kwa muda mrefu, hali ambayo itamnyima fursa ya kufaidi malove ya Mzambia huyo.
Hali ilikuwa ngumu zaidi kwa Msauzi wakati ulipowadia wakati wa kumuaga Maxwell ambapo Lerato alibadilika na kuonekana kukata tamaa. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti na Maxwell ambaye alionesha kukubali matokeo, ingawa naye alikuwa na majonzi kimtindo.
Lerato anakuwa na mshiriki wa pili kuachwa na mpenzi wake ndani ya Jumba la BBA, baada ya Kwaku wa Ghana kuachwa solemba na Merly wa Namibia, wiki moja kabla.
Usher Raymond avamiwa na chokoraa
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgzCnje4qKqJOYj2VihHKUXGy__gEu-2klWYY33x7s7Z8P-oZX0KbTGTzBVbgpaf8eFAj0qtJibPxOglpPALCZSw-NHpm7mCFCFh4Hh7JuvnkuemoHxHN11vwtMF1imQVk9ONoFZAG4l3SM/s200/usher+2.jpg)
Mexico City, Mexico
Ikiwa ni wiki chache tangu afunge ndoa, Staa wa R&B nchini Marekani, Usher Rymond, amekumbwa na bonge soo baada ya kuvamiwa na watoto wa mitaani chokoraa katika Jiji la Mexico nchini Mexico, alipokuwa matembezini.
Kwa mujibu wa magazeti ya udaku nchini Uingereza, msanii huyo alikwenda Mexico akiwa na mkewe, Tameka Fosta, ndipo alipovamiwa na watoto saba wa mitaani ambao walikuwa wakiomba msaada. Habari hizo zilieleza kuwa chokoraa hao, walimvamia Usher, wakiwa na uhakika wa kupata chochote kitu kutoka kwa mwana-R&B huyo.
Udaku huo ulinyetisha kuwa baada ya Usher kuona amezungukwa na watoto hao, aliwatuliza kwa kuwajaza mifuko, ndipo walitawanyika.
Mbali na kuwajaza noti, Usher aliwanunulia chokoraa hao chakula na vinywaji kwenye moja ya hoteli za matawi za juu jijini Mexico.
David Beckham atoa bonge la sapraizi
Los Angles, Marekani
Mchezaji wa Timu ya Soka ya Taifa la England, David Beckham, ametoa kauli ya kushangaza (sapraizi) kwa kueleza kuwa yeye ni mpezi mkubwa wa mchezo wa Rugby.
Becks alisema hayo, alipokuwa katika Uwanja wa Rugby, uliopo katikati ya Jiji la Los Angles, ikiwa ni jibu kwa waandishi wa habari waliomkuta akicheza mchezo huo.
Waandishi hao, walimuuliza Becks kama anacheza Rugby kwa mapenzi ama anaujua, kabla ya mwanasoka huyo anayekipika Klabu ya LA Galaxy ya Los Angeles, Marekani, kujibu kuwa mchezo huo anaupa chaguo la pili baada ya soka.
Napenda sana Rugby, mchezo huu unanivutia, isipokuwa soka ndiyo namba moja kwangu, mapenzi haya yanatoka moyoni.
''Kuna wakati huwa napata wazimu juu ya Rugby, ndiyo maana mnaona naucheza kwa nguvu zote'' alisema Becks.
Maisha ya Becks yapo Los Angeles tangu alipohamia Klabu ya Galaxy, Julai mwaka huu, akitokea Real Madrid ya Hispania.
Serena, Sharapova watemeana mbovu
Michigan, Marekani
Wacheza Tenisi maarufu duniani, Mmarekani Serena William (picha kubwa) na Mrusi Maria Sharapova, wiki iliyopita walitupiana maneno makali, walipokuwa kwenye bwawa la kuogelea lililopo Jimbo la Michigan, Marekani.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema, mastaa hao walifikia hatua hiyo baada ya Sharapova kutaka kuondoka mapema bwawani hapo, kwa madai kwamba alikuwa anawahi ndege ya kuelekea Jimbo la Xin Kian, China.
Ilielezwa kuwa kitendo hicho hakikumfurahisha Serena ambaye alichukulia hali hiyo kama nyodo kutoka kwa mdada huyo wa Kirusi, kwani hapo kabla alijua wangekuwa wote kwa siku nzima na kesho yake, wangesafiri pamoja kuelekea China.
Kwanza, Serena alimuuliza Sharapova, kulikoni kubadilisha ratiba ghafla? Inaoneka Shara alikuwa amedhamiria, kwani alisisitiza kuondoka, alipoona mwenzake habadili uamuzi, Serena alianza 'kumkoromea' Shara ambaye naye alijibu mashambulizi na kusababisha hali fulani ya vita ya maneno" alisema mmoja wa mashuhuda wa kijimgogoro cha mastaa hao.
![](file:///C:/DOCUME%7E1/user/LOCALS%7E1/Temp/moz-screenshot.jpg)
![](file:///C:/DOCUME%7E1/user/LOCALS%7E1/Temp/moz-screenshot-1.jpg)
![](file:///C:/DOCUME%7E1/user/LOCALS%7E1/Temp/moz-screenshot-2.jpg)