Thursday, November 15, 2007

Eto’o awazia CAN 2008

Barcelona, Hipania


Mshambuliaji wa Cameroon Samuel Eto’o anawazia michuano ijayo ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika nchini Ghana iwapo atakuwemo kwenye kikosi cha nchi hiyo au la.


Mshambualiaji huyo alisema kwamba japo hajui majaliwa yake katika michuano hiyo, lakini anawazia kulinda heshima ya Taifa lake katika michuano hiyo.


“Sijui lolote kama nitafanikiwa kucheza CAN ya nchini Ghana lakini mbivu na mbichi zitajulikana siku chache zijazo baada ya kurekebisha baadhi ya mambo yangu muhimu.

“Nitachokihitaji mimi ni kuona heshima ya nchi inaendelea kulindwa na kuwa juu kama miaka yote inavyokuwa kwa maana hili ndilo kila mtu analilia kufanyika katika taifa lake” Eto’o aliuambia mtandao wa Eurosport.


Mshambuliaji huyo amekuwa benchi kwa muda mrefu kwa sababu ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara jambo lilofanya viongozi wa juu wa Klabu ya Barcelona anayoichezea kusema wazi kwamba hawatamruhusu kucheza kwenye fainali zijazo za Ghana.

(Samuel Eto'o wa Cameron ambaye anawazia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana.)

Euro 2008

Vigogogo roho juu

(Fabio Cannavaro wa Italia)
(Rood Van Nistelrooy wa Uholanzi)




London, England

Vigogo wa soka Barani Ulaya hivi sasa vipo roho juu juu, kufuatia hofu ya kufuzu michuano ya Ulaya mwakani ‘Euro 2008’ kutokana na upinzani ulipo.

Kesho katika viwanja mbali mbali barani humo kutakuwa na michezo kadhaa ya kuwania tiketi ya kucheza michuano hiyo ambapo baadhi ya timu kubwa za soka barani humo zitakuwa vitani kuwania pionti tatu muhimu.

Katika mechi za kundi B, Scotland itakuwa na kibarua kigumu ikiwa nyumbani dhidi ya Italia ambayo pia ina nafasi nzuri ya kusonga mbele kama itafanya vizuri kwenye mchezo huo.

Nayo Israel ikiwa katika kundi E, itakuwa na kazi ya ziada kutetea ushindi wake wa nyumbani pale itakaposhuka dimbani ikipepetana na Urusi ambao wanaonekana kuwa na kikosi imara ambacho ni tishio katika kundi hilo.

Ujerumani ikiwa nyumbani itatakiwa kulinda heshima ya uwanja wa nyumbani kwani itahitaji ushindi wowote mbele ya Cyprus katika mchezo wa kundi D.

Vigogo wengine barani humo, Uholanzi nayo itataka kuonesha umwamba wake mbele ya washabiki wao watakapowakaribisha Luxembourg mchezo ambao unatabiriwa kuwa mgumu hivyo Wadachi hao hawatategemea mteremko katika mchezo huo, huku Slovakia watakuwa wageni wa ndugu zao wa Jamhuri ya watu wa Czech.

Katika michuano hiyo pia kutakuwa na mtanange wa kukata na shoka katika kundi A, pale Poland itakapoikaribisha Ubelgiji wakati mchezo mwingine wa kundi hilo utakuwa kati ya Kazakhstan wataokuwa wageni wa Serbia.

Mchezo wa kundi A ambao unatazamiwa kuwa mgumu zaidi ni pale Ureno itakaposhuka katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Armenia, wakati katika kundi F, shughuli itakuwa pevu pale Sweden watakapokaribishwa nyumbani kwa Hispania mchezo unaotarajiwa kuwa wa nguvu, hiyo ndiyo hali ilivyo katika michezo ya kufuzu Euro 2008.