Saturday, October 6, 2007

Umeipata hii ya waamuzi wa bongo?



Waamuzi safi lakini hawa mh!

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Simba Hassan Dalalali, alisema wazi kwamba kuna baadhi ya waamuzi wanaochezesha Ligi kuu Tanzania Bara, wamekuwa ni kikwazo kwa timu kadhaa kushindwa kufurukuta wanapokuwa kwenye viwanja vya Ugenini.

Inawezekana kauli ya Dalalali ikawa inaukweli fulani au ikawa haina ukweli wowote, lakini inalazimu kusema hayo kwa kuwa kuna baadhi ya viwanja huwa vinakuwa ni mwiba mchungu kwa timu ngeni.

Wote tunakumbuka Uwanja wa Ilulu ulioko mkoani Lindi ambao Timu ya Kariakoo ya mkoani humo ilikuwa ikiutumia kama uwanja wake wa Nyumbani.

Kumbu kumbu zinaonesha kwamba kati ya timu 10 zilizocheza katika uwanja huo ni timu tatu tu ambazo ziliweza kushinda ikimaanisha kwamba kati ya asilia 100 ya michezo yote iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ilulu ni asilimia 30 tu ambayo Kariakoo iliweza kufungwa.

Pia asilimia tano ndiyo pekee ambayo ilikuwa ni michezo ya sare huku asilimia iliyobakia ilikuwa Kariakoo ilishinda. Ushindi huo haukuwa na manufaa makubwa kwasababu bado timu hiyo ilikuwa ni kibonde katika ligi hadi kufikia kushuka daraja na kupotea katika anga ya soka kitaifa jambo lililodhihirisha wazi kuwa haikuwa na uwezo ila kinga yao kubwa ilikuwa ni waamuzi.

Lakini pia wakati Timu za Simba na Yanga zilipokuwa zinatumia Uwanja wa Taifa wa jijini Dar es Salaam, kulikuwepo na taarifa na malalamiko kutoka kwa timu za mikoani kwamba wenyeweji walikuwa wanapendelewa na waamuzi.

Kwa hali hiyo inaonesha wazi kuwa 'mchezo mchafu' unaokuwa unalalamikiwa na timu hizi kuwa zinaumizwa na baadhi ya waamuzi umekuwa umeshamiri na kuota mizizi kwa miaka nenda rudi hivyo kazi ya kuing'o itakuwa ni ngumu na inayohitaji muda lakini si jambo la leo na kesho kisha kupata kitu kilicho bora.

Madhara yanayofanywa na baadhi ya waamuzi ndiyo kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya soka nchini ni ukweli usiopingika kwamba maendeleo bora ya soka yanategemeo mengi ikiwemo waamuzi walio bora na wenye uwezo wa kufanya maamuzi bila kuyumbishwa na mtu au kikundi fulani.

Licha ya kuwepo kwa waamuzi wenye uozo na wababaishaji wakubwa lakini ukweli ni kwamba wapo wengine walio safi na wenye mwelekeo wa kusimamia ukweli pasipo kuyumbishwa na mtu wala kundi fulani.
Waamuzi wa aina hii ni mfano wa kuigwa na kila mpenda kandanda nchini kwani wao ndiyo muarobaini wa kuendeleza soka la Tanzania.

Tunajua kwamba wapo baadhi ya waamuzi ambao ni safi wasiokuwa na shaka, wanaosimamia ukweli hadi mwisho. Hawa ndiyo wanaaotakiwa katika kuhakikisha kwamba wanafanya soka la Tanzania linakuwa na mwelekeo unaoeleweka kwa manuaa ya sasa na baadaye.

Kuna kila sababu ya kulipongeza Shirikisho la Soka nchini TFF kufuatia kuchuakua uamuzi mzito wa kuwafungia waamuzi kadhaa walioonekana kwamba ni kikwanzo katika maendeleo ya soka kwenye Taifa letu.

Hali hii ilikuwa ni moja ya njia ya kuhakikisha kwamba waamuzi wanaopewa dhamana ya kusimamia Ligi Kuu mwaka huu wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za soka.

TFF ilikuwa na kila sababu ya kusimamia ukweli huo kwa ajili ya kuinusuru hali ya soka la Tanzania lakini, hili si halitoshi pia kinachotakiwa ni kufanya usafi kwenye sekta ya waamuzi kwa mara nyingine ili kujisafuisha zaidi.



Huyu ndiye The Bossss pale Ikulu ya soka nchini Tanzania anaitwa Frederick Mwakalebela a.k.a Katibu Mkuu wa TFF.

Si hilo pekee lakini jambo lingine linalotakiwa kuangaliwa ni wenyewe TFF kama kuna baadhi ya vigogo wasiokuwa waamini ambao kwa namna moja amba nyingine wamekuwa wakishinikiza kwa timu fulani kuwa na matokeo ya anayotaka yeye ambalo si sahihi.

Itakuwa ni aibu kubwa kama shirikisho ambalo ndilo baba wa soka nchini, ikitokea kiongozi mmoja wa viongozi wa juu wa TFF, aanze kufanya hujuma za kupanga matokeo kwenye baadhi ya mechi ili aweze kunufaika kwa maslahi anayoyajua yeye.

Kinachotakiwa ni kwamba timu ziachwe ziamue zenyewe kulingana na uwezo wa timu husika. Kama timu uwezo wake ni mdogo basi zikubaliane na matokeo na zile zenye uwezo mkubwa ziachwe zipete. Mano mzuri tumeshuhudia vigogo wa soka la Bongo Simba na Yanga zikiwa zimelala ama kuambulia sare.

Haya ni matokeo yanayotoa changamoto kwa vigogo hao kwa kuwa wamekuwa hawaandai timu kwa kiwango kinachotakiwa bali wanakuwa wakijitutumua na kutumia mamiloni ya shilingi kununua wachezaji kutoka nje ya nchi ambao wengi wameshazeeka na wanashindwa kuendana na kasi ya wachezaji chipukizi waliopo katika baadhi ya timu.

Mambo haya ndiyo ambayo yanazikumba timu hizi kila mwaka kwa maana hazina utamaduni wa kuwa na kikosi kilichojengeka wa muda mrefu bali zinekuwa zikisajili wachezaji wapya kila mwaka hivyo kufanya walimu kuwa na kazi ya kusuka kikosi kipya kila mwaka.

Vile vile kwa upande wa benchi la ufundi la timu hizi limekuwa halidumu bali kila kukicha utakuta watu wanabadishwa na kuwekwa watu wapya huku wakifiri kwamba chanzo cha timu zao kufanya vibaya ni benchi la ufundi na kushindwa kuelewa dawa sahihi ya kuponya ugonjwa wao ilikuwa ni Panaldo na si Muarobaini kwani kinachotakiwa ni kuwa na kikosi cha muda mrefu.

Lazima kila mtu aelewe kwamba Tanzania inahitaji kuona timu zinashinda kulingana na uwezo wake na si kutegemea nguvu ya refa ili kuwa na bingwa mwene uwezo na si bora bingwa.

Tunataka bingwa mwenye uwezo wa kuwawakilisha vyemna watanzania zaidi ya milioni 34 ambao wengine wanazaliwa hadi wakati huu tunavyozunyumza. Vita ni ngumu lakini TFF tuliwakabidhi silaha za aina zote ili kuhakikisha kwamba tunaibuka washindi katika vita hii muhimu kwa nchi hetu, huo ndiyo moyo wa kizalendo unaotakiwa kufuatwa na kila Mtanzania na asiye Mtanzania.


HII NI EXCLUSIVE NEWS KUTOKA PALE MITAA YA Jangwani na Twiga almaarufu kama Yanga.


Mpoland kuinoa Yanga Kaunda









Wojciech Lazarek akiwa katika picha tofauti(picha kwa hisani ya mtandao wa Gooogle)



KOCHA mpya wa Yanga kutoka nchini Poland, Wojciech Lazarek, ataanza kuifundisha timu hiyo katika Uwanja wa Kaunda uliopo Makao Makuu ya Klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.


Habari kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo zilidhibitishwa na mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga, zilisema kwamba Lazarek huenda akautumia Uwanja huo baada ya ukarabati wake kukamilika kwa asilimia 40.

Kiongozi huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema juhudi za makusudi zinafanyika ili kuhakikisha ujenzi wa Uwanja wa Kaunda unakwenda haraka ili Lazarek akitua aukute ukiwa tayari ama katika hatua za mwisho.

"Kama mlivyotangaziwa kwamba Kocha Lazarek, atatua mapema Oktoba 12, mwaka huu na baada ya kumalizana naye atarejea nchini kwao kwa ajili ya kuchukua vifaa vyake na baadaye kurejea kuinoa Yanga.

"Wakati huo sisi tutajitahidi uwanja wetu uishe mapema ili timu iwe inafundishwa hapa hapa lengo likiwa kumwezesha kocha wetu kufanya kazi kirahisi lakini kubwa kuliko yote ni kupunguza matumizi kwa kulipia viwanja vya nje ya klabu," alisema Kiongozi huyo.

Kocha Lazarek (69) alitangazwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Yanga Imani Madega, kuwa ndiye atakayechukua nafasi ya Mserbia Milutin Sredojevic 'Micho'(37) ambaye alibwaga manyanga mara baada ya Ligi Ndogo ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kumalizika.

Naye Mweka hazina wa klabu hiyo, Abeid Abeid 'Falcon' alisema kuwa suala la ujenzi huo linakwenda vizuri kama lilivyopangwa na hivi sasa wapo katika hatua ya tatu ambayo ni kuweka mchanga maalum kwa ajili ya kuzuia magugu kuota.

Falcon aliongeza kuwa mbegu za kupandwa uwanjani hapo zinatarajia kuwasili wakati wowote kuanzia sasa zikitokea nchini Afrika Kusini, baada ya shughuli za awali kukamilika na kwamba zitaoteshwa kwa siku 20 tu.

Yanga mishoni mwa wiki iliyopita ilishinda ikiwa ni mchezo wa pili tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera. Matokeo hayo yanakuja ikiwa ni siku chache tangu Uongozi kuunda kamati ya ushindi iliyowahusisha Francis Kifukwe, Baraka Igangula na Jamal Malizi waliokuwa viongozi wa zamani wa klabu hiyo kubwa nchini.