Na Ahadi Kakore
KWANZA napenda nimshukuru Mungu muweza wa yote kwa wema na fadhila zake kwangu, hasa kwa kuniwezesha kufika wakati huu, nawajibika kusema hayo kwa sababu wapo wengi tuliokuwa nao siku, saa na dakika chache zilizopita lakini leo hii hawapo nasi tena.
Vile vile naomuomba Mwenyezi Mungu anijalie hekima ya kutosha na kuniwezesha kuandika yanayostahili katika uchambuzi huu ili ujumbe ufike kama nilivyokusudia, naamini sala yangu imesikika.
Baada ya kusema hayo, nirejee kwenye kiini cha mjadala, ambapo siku ya Jumatano wiki iliyopita Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega akiwa sambamba na Mhazini wao, Abeid Mohamed Abeid 'Falcon' pamoja na Katibu Mwenezi, Francis Lucas walilazimika kuitisha mkutano na wahariri wa vyombo vya habari za michezo nchini.
Mkutano huo uliitishwa na viongozi hao baada ya aliyekuwa mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji kutangaza kujitoa kwenye ufadhili wake ndani ya klabu hiyo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Manji alieleza kuwa sababu za kujitoa ni kutokana na viongozi wa Yanga kushindwa kutekeleza rasimu ya katiba kama walivyokubaliana awali.
Lakini baada ya kutangaza kujiondoa ndani ya Yanga, siku iliyofuata alirejea Jangwani akiwa ameambatana na kundi la wazee na baadhi ya wanachama. Hatua hiyo ilikuja baada wazee kumuangukia.
Katika mkutano huo na wahariri, Madega alifafanua kuwa mbegu ya kutoelewana na Manji ilianza kumea wiki moja baada ya kuchaguliwa kwao, baada ya mfadhili huyo kukutana na viongozi na kuwaeleza hatua ya kusaini mkataba ambao ungeifanya timu iwe chini ya Kampuni badala ya klabu.
Mageda alisema yeye hakukubaliana na hatua hiyo, tofauti na viongozi wengine "Binafsi nilihamaki sana kwa kuwa ninaamini mimi ni mtu mzima mwenye akili timamu, msomi na nina uwezo wa kawaida wa kuchanganua mambo na zaidi kitaalam mimi ni mwanasheria.
"Nalinda heshima yangu zaidi kuliko maslahi, hivyo kwa uwazi kabisa sikukubali kufanya vile, kama kiongozi mkuu hadi hapo katiba ya Yanga pamoja na muafaka wenyewe nitakapoupitia kikamilifu," ilisema taarifa ya Madega aliyoitoa.
Kadhalika taarifa hiyo ilisema kwamba katika katiba kuna upungufu kadhaa ambao ni muhimu kufanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa mchakato wa kampuni.
Alifafanua baadhi ya vifungu vya katiba, kiwemo cha 39 (2) (d) kuwa kinauagiza mkutano mkuu wa uchaguzi, kuchagua wanachama wawili ambao si miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu katika kampuni.
Hivyo akasema kifungu hicho na vingine havina budi kufanyiwa marekebisho makubwa kabla ya kukubali kujitumbukiza katika kampuni.
Hayo yaliyosemwa na Mageda yawezekana yakawa na ukweli lakini naamini haikuwa kauli ya kukurupuka kwa sababu anaelewa madhara ya kufanya mambo kwa kukurupuka akiwa kama kiongozi mkubwa.
Kwa upande wa pili wa shilingi, tumeshuhudia Manji akijitoa huku akisisitiza kwamba hali ya mambo ilivyo hivi sasa ndani ya Yanga ndiyo yaliyosababisha kujiondoa kwake lakini akisisitiza kwamba rasimu ya katiba imekuwa haifuatwi.
Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuondokewa na mfadhili, kwani mwaka 1994, ilikimbiwa na wafadhili watano akiwemo Marehemu, Abbas Gulamali, wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa George Mpondela 'Castro'.
Ikumbukwe kwamba wakati Manji anaingia ndani ya Yanga kulikuwa na mgogoro mkubwa ambao watu mbali mbali walishindwa kuuzima. Mgogoro huo ulidumu kwa muda wa zaidi ya miaka mitano na kusababisha maendeleo ya klabu hiyo kuwa duni licha ya kwamba iliwahi kuibuka ubingwa ndani ya kipindi hicho.
Ni ukweli usiofichika kwamba pamoja na mataji yaliyopatikana katika wakati huo lakini mgawanyiko uliokuwepo uliigawa Yanga katika makundi matatu ambayo ni Asili, Academia na Kampuni.
Kutua kwa Manji mitaa ya Twiga na Jangwani kulisababisha mgawanyiko uliokuwepo kumalizika na kupatikana Yanga moja imara, sambamba na hilo kulifanyika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo mwezi Mei mwaka huu na kuwaweka madarakani viongozi waliopo hivi sasa.
Hali hiyo inanifanya kufunua Biblia Takatifu na kukutana na ujumbe kutoka katika kitabu cha Zaburi 125:4 ambao unasema "Ee Bwana, uwatendee mema walio wema, nao walio wanyofu wa moyo".
Kwa upande wa Quruan Tukufu inasema "Innal hilah maswabirina' ikiwa na maana ya 'Hakika wenye kusubiri wapo pamoja na Mwenyezi Mungu'.
Kwa maana hiyo hoja zilizotolewa na pande zote mbili zinafaa kuchujwa na kutazamwa kwa macho mawili ili kumuondoa Bundi mbaya anayeweza kuifikisha klabu pabaya.
Nimeamua kutumia vifungu kutoka katika vitabu hivi kwa sababu binafsi naamini moja ya kitabu hicho lakini pia wengine wanaamini vitabu hivi katika maisha yao ya kila siku.
Hatukuzoea kuona wachezaji wa Yanga wakijihusisha na mgogoro ndani ya klabu, lakini kwa kipindi hiki tumeshuhudia yanatokea jambo ambalo ni hatari, kwani awali timu ikiwa ndani ya migogoro ilikuwa inatwaa vikombe kwa sababu wachezaji walikuwa wakijiepusha nayo.
Wito wangu kwa Wanayanga wote ni nawaomba wote wanaohusika na sakatala hili kuweka tofauti zao chini na kuangalia mbele kwa manufaa ya Yanga.
=========================================================
Vimbwanga vya mastaa
Rais asiyecheka Duniani
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj3eSWxmXME7vDeGu9-Ngpj_dXGwCihTHFM8Bie_yPi7v9UJpL0TJb90M5BbiyV1TVfWC_QlqbUEOR5j81k0ZWrf66E2af5mhu5islI4a8cMbJR5IFiqvz6YaAEYye4TAQOEIEJ_kanTWoi/s200/rais+wa+Korea+kaskazini.jpg)
Pung Yang, Korea Kaskazini
Rais wa Jamhuri ya watu wa Korea Kaskazini, Kim Jong-il anasemekana kuwa ndiye kiongozi asiyependa kucheka ikilinganishwa na viongozi wengine duniani.
Kwa mujibu wa jarida moja la nchini humo,Kim Jong-il akiwa amefurahishwa na jambo huishia kutikisa kichwa au kunyanyua mikono na kuwapungia wananchi wake.
Imefahamika kwamba Kiongozi huyo anayefuata mlengo wa Kimonisti, amekuwa na tabia hiyo kwa muda mrefu jambo linalowafanya watu wengi ambao si raia wa nchi hiyo kushindwa kutambua wakati gani huwa na furaha.
Wachunguzi wa mambo wanadai kwamba watu wengi waishio nchini humo wameshindwa kufanikiwa kuyaona 'meno' ya kiongizi wao japo hata kwa bahati mbaya, jambo linalowafanya watu wengi kumwogopa.
Viongozi wa kijeshi nchi humo ndio waliobahatika kumwona Kim Jong-il akicheka kwa mara ya mwisho wakati alipotembelea kituo kimoja cha kijeshi nchini humo kushuhudia majaribio ya makombora ya masafa marefu jambo ambalo lililaaniwa Marekani.
=========================================================
Mapenzi yamchanganya Michel Jackson
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgkfoY5krIoZjvHQFwwfm88RjrKkFMmXBRgWcvxu262TPToYxo2G69JCZuV1SXaYIDcaVKmvL3SYAl9vknfrB63diQeURd7a6M3aSR7uotxNTRVT3xODVS-npjJuIkc-97bJnQ-__uxHdMG/s200/SNN0633B_280_367627a.jpg)
Califonia, Marekani
Mwanamuziki wa miondoko ya Pop duniani, Michael Jackson, ameweka wazi kwamba mapenzi aliyopata kutoka kwa mfanyakazi wake wa ndani 'yaya' yalimdatisha.
Jackson alisema kwamba mwanadada Rose, alikuwa anampa mapenzi moto moto ambayo yalimchanganya kiasi kwamba alianza kufikiria namna ya kufunga naye ndoa.
"Ukweli Rose alinidatisha sana na penzi lake hilo halina ubishi, kiasi cha kufikia hatua ya kutaka kufunga naye ndoa wakati fulani japo haikufanikiwa, huo ndio ukweli wa uhisiano wangu na Rose" alisema Jackson.
Siku za nyuma iliwahi kuripotiwa kwamba, Jackson alikuwa akiwekwa kinyumba na mfanyakazi wake wa ndani, jambo alilolikanusha vikali na kuwakasirisha majirani zake waliokuwa wakidai Jackson alikuwa akiukataa ukweli.
=========================================================
J.Lo afuata nyayo za Madona
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhYDwSwnrLJXNrPsFfomWEjH6O3ut6M_XfLdWaBNLVceMdskIa_1auYFkUolJCkBaj5dLMwUocV6jNI42NOWlkJuip81fwezRIC5DVezjshLy0P1DOSbUgjnEJDsaPVxsPWRsbMllVBC7tg/s200/jennifer-lopez-.jpg)
Alabama, Marekani
Mwanamuziki nyota wa R&B nchini Marekani Jenifer Lopez, amesema kwamba kama yupo mbioni kufuata nyayo za mwanamuziki mwenzake, Lady Madona.
Akizungumza katika kituo kimoja cha Luninga katika jimbo la Alabama nchini Marekani, Lopez 'J.Lo' alisema kwamba Madona ndiye mwanamuziki ambaye anamvutia kutokana na mtindo wa maisha yake wa kulea watoto wenye matatizo.
"Hata mimi nikifanikiwa kuweka mambo yangu sawa nitafanya kama alivyofanya Madona, wakati huu najipanga kwa ajili ya kuchukua watoto wawili ili niishi nao kama watoto wangu hili linawezekana" alisema J.Lo.
Madona alimchukua David Banda wa nchini Malawi kwa ajili ya kumlea kama mwanaye, lakini bado haijafahamika J.Lo atawachukua watoto kutoka sehemu gani duniani.
=========================================================
Rihanna; nasakwa usiku na mchana
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgxpk0BL17ninjNHDx6WZR-hMoNCMALhEtL5w3Fu5HcJzHW_AbFyfvs51kez4Oi4abaqZuL-RVZTexFNbjs4yWvZTsblqKC-IlNNyCS_Aa-mzuW5C1Na6vb7VFaHZt0O686-iMBpuECRL1A/s200/rihanna_5.jpg)
London, Uingereza
Mwanamuziki Rihana wa Marekani aliyejipatia umaarufu katika miondoko ya R&B amesema kwamba anasakwa na wanaume wakware usiku na mchana ili kufanya nao ngono.
Msanii huyo alisema hayo wakati alipoulizwa na gazeti la The Sun la nchini Uingereza, ni kitu gani kinachomsumbua katika maisha yake ya ustaa.
"Maisha ya Ustaa ni tabu tupu hakuna asiyefahamu haya, mambo yanayonisumbua ni wanaume wanaonitafuta ili kufanya nao ngono" alisema Rihana.
Msanii huyo aliongeza kwamba pamoja na mambo mengine lakini maisha ya aina hiyo ni magumu kwani anafuatiliwa sana, vikiwemo vyombo vya habari ambavyo kila siku vinataka kujua undani wa maisha yake.