Sunday, December 16, 2007

Unajua kilichotokea katika tuzo ya mwanasoka bora wa dunia wa gazeti la Championi mwaka 2008.


Mratibu wa shindano la mwanasoka bora wa mwaka wa gazeti la Championi 2007, Ahadi Kakore (katikati) akitangaza matokeo ya shindano hilo mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni, kushoto ni Mhariri Isaac Kijoti na kushoto ni mhariri Denis Fusi.

Friday, November 16, 2007

Wachezaji England wamkaanga McClaren

Kocha wa Timu ya Taifa ya England, Steve McClaren akisisitiza jambo kwa wachezaji. (Picha kwa hisani ya mtandao wa chama cha soka cha England FA.)

London, England

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya England wamemkaanga Kocha Mkuu wa timu hiyo, Steve McClaren baada ya kusema wazi kuwa hawawezi kupigana kwa ajili ya kutetea kibarua cha kocha wao.

Wachezaji hao wamesema kwamba licha ya umuhimu wa kufuzu mchezo ujao dhidi ya Crotia lakini hawatacheza kwa nje ya uwezo wao ili kulinda kibarua cha McClaren japo watajitahidi ili lengo la kulinda heshima ya nchi litimie.

Pia walisema kwamba hawatachukua jukumu la kuomba chama cha soka nchini humo (FA) ili McClaren aendelee kuinoa timu hiyo kwa sababu kile ambacho wapenda soka walihitaji hajakifanya.

Michael Owen alisema:Hatuwezi kubebena kiasi hiki lakini tunakachokifanya ni kulinda heshima ya nchi na si heshima ya mtu mmoja mmoja."

Naye Steven Gerrard alisema kwamba: Lakini jambo la msingi ni kulinda heshima ya Waingereza mbele ya mashabiki wa soka kote Ulimwenguni"

“Inajulikana wazi kuwa jukumu la timu kushinda halipo kwa wachezaji pekee, lakini kocha ana nafasi yake hivyo kama ameshindwa kutekeleza kile kinachotakiwa ni lazima awajibike kama ambavyo mtu mwingine anaweza kuwajibika akifanya isivyotarajiwa na wengi." alisema Peter Crouch.

England inakabiliwa na kibarua kigumu wakati itakapocheza na timu ya Taifa ya Crotia ikiwa ni moja ya mchezo wa kufuzu katika michuano ya Euro mwakani lakini ikiwa katika wakati mgumu wa kufuzu ikilinganishwa na timu nyingine kutoka katika kundi hilo ambazo ni Ujerumani, Israel, na Croatia.

Wigan yamlilia Bruce

London, England

Mwenyetiki wa klabu ya Wigan Athletic, Dave Whelan amesema kwamba anasubiri majibu kutoka kwa klabu ya Birmingham City kufuatia ombi la kumtaka Kocha Steve Bruce.

Whelan alisema kwamba Kocha huyo ameonesha mafanikio na watafanya kila liwezekalano ili Bruce anatua kwenye klabu hiyo.

“Tumeangalia kwa makini na tumegundua kwamba kuna uwezekano wa kufanya vizuri kama alivyofanya akiwa na Birmingham City hili ndilo linalotuumiza vichwa” Whelan aliliambia shirika la habari la Uingereza BBC.

Steve Bruce (46) anasakwa kwa udi na uvumba na tajiri wa Wigan Athletic raia wa Hong Kong, Carson Yeung ili kurejeshwa kuinoa Wigan Athletic.
.

Thursday, November 15, 2007

Eto’o awazia CAN 2008

Barcelona, Hipania


Mshambuliaji wa Cameroon Samuel Eto’o anawazia michuano ijayo ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika nchini Ghana iwapo atakuwemo kwenye kikosi cha nchi hiyo au la.


Mshambualiaji huyo alisema kwamba japo hajui majaliwa yake katika michuano hiyo, lakini anawazia kulinda heshima ya Taifa lake katika michuano hiyo.


“Sijui lolote kama nitafanikiwa kucheza CAN ya nchini Ghana lakini mbivu na mbichi zitajulikana siku chache zijazo baada ya kurekebisha baadhi ya mambo yangu muhimu.

“Nitachokihitaji mimi ni kuona heshima ya nchi inaendelea kulindwa na kuwa juu kama miaka yote inavyokuwa kwa maana hili ndilo kila mtu analilia kufanyika katika taifa lake” Eto’o aliuambia mtandao wa Eurosport.


Mshambuliaji huyo amekuwa benchi kwa muda mrefu kwa sababu ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara jambo lilofanya viongozi wa juu wa Klabu ya Barcelona anayoichezea kusema wazi kwamba hawatamruhusu kucheza kwenye fainali zijazo za Ghana.

(Samuel Eto'o wa Cameron ambaye anawazia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana.)

Euro 2008

Vigogogo roho juu

(Fabio Cannavaro wa Italia)
(Rood Van Nistelrooy wa Uholanzi)




London, England

Vigogo wa soka Barani Ulaya hivi sasa vipo roho juu juu, kufuatia hofu ya kufuzu michuano ya Ulaya mwakani ‘Euro 2008’ kutokana na upinzani ulipo.

Kesho katika viwanja mbali mbali barani humo kutakuwa na michezo kadhaa ya kuwania tiketi ya kucheza michuano hiyo ambapo baadhi ya timu kubwa za soka barani humo zitakuwa vitani kuwania pionti tatu muhimu.

Katika mechi za kundi B, Scotland itakuwa na kibarua kigumu ikiwa nyumbani dhidi ya Italia ambayo pia ina nafasi nzuri ya kusonga mbele kama itafanya vizuri kwenye mchezo huo.

Nayo Israel ikiwa katika kundi E, itakuwa na kazi ya ziada kutetea ushindi wake wa nyumbani pale itakaposhuka dimbani ikipepetana na Urusi ambao wanaonekana kuwa na kikosi imara ambacho ni tishio katika kundi hilo.

Ujerumani ikiwa nyumbani itatakiwa kulinda heshima ya uwanja wa nyumbani kwani itahitaji ushindi wowote mbele ya Cyprus katika mchezo wa kundi D.

Vigogo wengine barani humo, Uholanzi nayo itataka kuonesha umwamba wake mbele ya washabiki wao watakapowakaribisha Luxembourg mchezo ambao unatabiriwa kuwa mgumu hivyo Wadachi hao hawatategemea mteremko katika mchezo huo, huku Slovakia watakuwa wageni wa ndugu zao wa Jamhuri ya watu wa Czech.

Katika michuano hiyo pia kutakuwa na mtanange wa kukata na shoka katika kundi A, pale Poland itakapoikaribisha Ubelgiji wakati mchezo mwingine wa kundi hilo utakuwa kati ya Kazakhstan wataokuwa wageni wa Serbia.

Mchezo wa kundi A ambao unatazamiwa kuwa mgumu zaidi ni pale Ureno itakaposhuka katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Armenia, wakati katika kundi F, shughuli itakuwa pevu pale Sweden watakapokaribishwa nyumbani kwa Hispania mchezo unaotarajiwa kuwa wa nguvu, hiyo ndiyo hali ilivyo katika michezo ya kufuzu Euro 2008.

Friday, November 9, 2007

Kombe la Dunia 2014 litafunika-Pele

Huyu ndiye yule mfalme wa soka Duani, Edson Arentes do Nascimento 'Pele'


Brasilia, Brazil

Mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Brazil, Edson Arentes do Nascimento maarufu kama Pele, amesema kwamba michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2014, 'itafunika' itavunja rekodi ya michuano mingine iliyopita.

Pele amesema kwamba atatumia uwezo wake wote kuhakikisha kwamba anaitangaza Brazil katika kipindi chote cha maandalizi ya michuano hiyo ambayo mwaka 2014 itafanyika nchini Brazil.

"Michuano ya 2014 itavunja rekodi, kwani haijawahi kutokea kamwe, mimi kama balozi, nitaitangaza nchi yangu kwa nguvu zote na kushirikiana bega kwa benga na serikali, shirikisho la soka la Brazil 'CBF' pamoja na wadau wengine humihu ili kuweka mambo sawa kabla ya kuanza kwa michuano." Alisema Pele.

Brazil hivi karibuni ilisema kwamba, itawatumia wanasoka wake wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya pamoja na wale waliostaafu siku nyingi akiwemo Pele, ili kuitangaza nchi hiyo kimataifa zaidi.

Mshike mshike Klabu bingwa barani Ulaya 2007

Man United, Barca zaua,
Arsenal yapaa Ronaldo,
Rooney, Tevez wameremeta






London England


Kivumbi cha Ligi ya mabingwa barani Ulaya kiliendelea tena, usiku wa kuamkia jana katika viwanja mbalimbali ambapo timu ya Manchester United, ikiwa nyumbani ilipata ushindi mnono baada ya kuitandika Dynamo Kiev bao 4-0.


Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Old Trafford, ambapo makosa yaliyofanywa na walinzi wa Dynamo yalisababisha kuleta zahama kwa timu hiyo, baada ya mchezaji wa Manchester United, Pique kuandika bao la kwanza katika dakika ya 31 ya mchezo.


Bao hilo liliongeza hamasa ya mashambulizi kwa Manchester United, jambo lililofanya washambuliaji wake kama Cristiano Ronaldo na Wayne Rooney, kutumia makosa madogomadogo hivyo kuongeza bao la pili lililofungwa na Carlos Tevez katika dakika ya 37. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Manchester United ilikuwa mbele kwa bao 2-0.


Katika kuonesha kwamba mwaka huu Mashetani Wekundu hao, walikuwa na uchu wa kufika mbali, Wayne Rooney aliwanyanyua tena mashabiki wake kwenye viti, baada ya kuandika bao la tatu katika dakika ya 76.


Pamoja na ushindi huo mnono lakini haikutosha kwani Mreno Cristiano Ronaldo, alihitimisha karamu ya mabao kwa Machester United, baada ya kufunga bao la nne katika dakika ya 88. Hivyo hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa Manchester United bao 4 na Dynamo Kiev 0.


Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, timu ya Barcelona ya Hispania ilitoka na ushindi mnono wa bao 2-0 dhidi ya Rangers, mchezo ambao Barca ndio walikuwa wenyeji.

Bao la kwanza kwa upande wa Barcelona lilipatikana katika dakika ya saba ya mchezo, kupitia kwa mshambuliaji mwenye kasi, Thierry Henry.

Mchezo huo uliendelea huku Barca wakiwa wapo juu, kuliko wageni wao jambo lilifanya mchezo kuelemea upande mmoja, licha ya kwamba kulikuwa na mashambulizi ya kustukiza langoni kwa Barcelona.

Hali hiyo ilimlazimisha Kocha wa timu hiyo, Frank Rijkaard kusimama na kuhamasisha vijana wake na kusababisha kupatikana bao la pili, kupitia kwa Lionel Messi aliyefunga katika dakika ya 43 ya mchezo akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mbrazil Ronaldinho Gaucho.

Pamoja na matokeo hayo lakini kulikuwa na mchezo mwingine, ambapo timu ya Lyon ikiwa nyumbani ilitoka na ushindi mnono wa bao 4-2 dhidi ya timu ya Stuttgart.

Mabao ya Lyon yalifungwa na Ben Arfa katika dakika ya sita na 37, hivyo kuonekana kwamba kulikuwa na matumaini mapya ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Naye mchezaji Källström aliifungia Lyon bao la pili katika dakika ya 15 ya mchezo, wakati dakika ya 90 ya mchezo Juninho alifunga mlango wa mabao kwa timu yake baada ya kuandika bao la nne.

Licha ya Lyon kupata mabao hayo lakini Stuttgart Gomez ilijitutumua na kuandika mabao mawili ya kufutia machozi yaliyoandikwa na Gomez katika dakika ya 16 na 56.

Wakati huo huo Slavia Praha ilishindwa kutamba nyumbani na kuruhusu kugawana pointi na Arsenal, hivyo matokeo ambayo yaliwezesha watoto Mfaransa Arsene Wenga kupata kupita na kutua hadi kwenye hatua ya mtoano.

Wakati hayo yakiendelea lakini kwa upande wa Kocha wa Liverpool, Rafael Benitez amesema kwamba, baada ya kutoa kipigo cha Mbwa mwizi kwa baada ya kuichapa Besiktas ya Uturuki kwa bao 8-0, anaangalia ni vipi ataweza kuifunga Futebol Clube do Porto, maarufu kama FC Porto ya Ureno wakati, huku vijongoo hao wa Anfield watakapokuwa ugenini katika Uwanja wa Estádio do Dragão jijini Lisbon Ureno. Mchezo huo baina ya FC Porto na Liverpool utashudiwa na mashabiki wapatao 50,476.