Man United, Barca zaua,
Arsenal yapaa Ronaldo,
Rooney, Tevez wameremeta
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgPOp8CgUm10SEbey5uLtgUcr5lBDTlAFaqNUvcqBUOAQFJ0xj3QAwqQCv3UfgHpynT-YXDjUzq7_sHg7Md9Rqe8z5kK2XPILMMowXa1R_waRKd-QS8wYZ1YuWhogLqu1PELzyQhvvToHwN/s400/WayneRooneyBrilliant_000.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiVKH7xEtnuDe4SlMPZRYm2a-f8myOFn5uLpetS6RURbhQctghyphenhyphenBnhlXFAYIR6UNMSkwvrAN9Y03UwUpOkzKZSLMXuCZafeGbhCZ_DVBg6eeEk1T2fk5iWFqd-OwUfPyUZZySzMSJQzF3MW/s400/wenger.jpg)
London EnglandKivumbi cha Ligi ya mabingwa barani Ulaya kiliendelea tena, usiku wa kuamkia jana katika viwanja mbalimbali ambapo timu ya Manchester United, ikiwa nyumbani ilipata ushindi mnono baada ya kuitandika Dynamo Kiev bao 4-0.
Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Old Trafford, ambapo makosa yaliyofanywa na walinzi wa Dynamo yalisababisha kuleta zahama kwa timu hiyo, baada ya mchezaji wa Manchester United, Pique kuandika bao la kwanza katika dakika ya 31 ya mchezo.
Bao hilo liliongeza hamasa ya mashambulizi kwa Manchester United, jambo lililofanya washambuliaji wake kama Cristiano Ronaldo na Wayne Rooney, kutumia makosa madogomadogo hivyo kuongeza bao la pili lililofungwa na Carlos Tevez katika dakika ya 37. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Manchester United ilikuwa mbele kwa bao 2-0.
Katika kuonesha kwamba mwaka huu Mashetani Wekundu hao, walikuwa na uchu wa kufika mbali, Wayne Rooney aliwanyanyua tena mashabiki wake kwenye viti, baada ya kuandika bao la tatu katika dakika ya 76.
Pamoja na ushindi huo mnono lakini haikutosha kwani Mreno Cristiano Ronaldo, alihitimisha karamu ya mabao kwa Machester United, baada ya kufunga bao la nne katika dakika ya 88. Hivyo hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa Manchester United bao 4 na Dynamo Kiev 0.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, timu ya Barcelona ya Hispania ilitoka na ushindi mnono wa bao 2-0 dhidi ya Rangers, mchezo ambao Barca ndio walikuwa wenyeji.
Bao la kwanza kwa upande wa Barcelona lilipatikana katika dakika ya saba ya mchezo, kupitia kwa mshambuliaji mwenye kasi, Thierry Henry.
Mchezo huo uliendelea huku Barca wakiwa wapo juu, kuliko wageni wao jambo lilifanya mchezo kuelemea upande mmoja, licha ya kwamba kulikuwa na mashambulizi ya kustukiza langoni kwa Barcelona.
Hali hiyo ilimlazimisha Kocha wa timu hiyo, Frank Rijkaard kusimama na kuhamasisha vijana wake na kusababisha kupatikana bao la pili, kupitia kwa Lionel Messi aliyefunga katika dakika ya 43 ya mchezo akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mbrazil Ronaldinho Gaucho.
Pamoja na matokeo hayo lakini kulikuwa na mchezo mwingine, ambapo timu ya Lyon ikiwa nyumbani ilitoka na ushindi mnono wa bao 4-2 dhidi ya timu ya Stuttgart.
Mabao ya Lyon yalifungwa na Ben Arfa katika dakika ya sita na 37, hivyo kuonekana kwamba kulikuwa na matumaini mapya ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Naye mchezaji Källström aliifungia Lyon bao la pili katika dakika ya 15 ya mchezo, wakati dakika ya 90 ya mchezo Juninho alifunga mlango wa mabao kwa timu yake baada ya kuandika bao la nne.
Licha ya Lyon kupata mabao hayo lakini Stuttgart Gomez ilijitutumua na kuandika mabao mawili ya kufutia machozi yaliyoandikwa na Gomez katika dakika ya 16 na 56.
Wakati huo huo Slavia Praha ilishindwa kutamba nyumbani na kuruhusu kugawana pointi na Arsenal, hivyo matokeo ambayo yaliwezesha watoto Mfaransa Arsene Wenga kupata kupita na kutua hadi kwenye hatua ya mtoano.
Wakati hayo yakiendelea lakini kwa upande wa Kocha wa Liverpool, Rafael Benitez amesema kwamba, baada ya kutoa kipigo cha Mbwa mwizi kwa baada ya kuichapa Besiktas ya Uturuki kwa bao 8-0, anaangalia ni vipi ataweza kuifunga Futebol Clube do Porto, maarufu kama FC Porto ya Ureno wakati, huku vijongoo hao wa Anfield watakapokuwa ugenini katika Uwanja wa Estádio do Dragão jijini Lisbon Ureno. Mchezo huo baina ya FC Porto na Liverpool utashudiwa na mashabiki wapatao 50,476.